Malumbano kuhusu umiliki wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) yaliendelea jana Bungeni ambapo wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walituhumiana kuhongwa na pande mbili zinazogombea kumilikishwa shirika hilo.
Kulitokea mabishano kati ya Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Athuman Kapuya na Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu, ambao kila mmoja alimtuhumu mwenzake kuhongwa ili kufanikisha umilikishwaji wa shirika hilo kongwe, ambalo sasa hivi linaendeshwa na Kampuni ya Simon Group.
Mapambano hayo ya maneno makali yaliibuka wakati wabunge wakijadili hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Uchumi ya mwaka 2014/15.
Akitoa mchango wake, Mtemvu alikuwa wazi kwa kuwatubumu Profesa Kapuya na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, kuwa walihusika moja kwa moja katika uuzaji wa shirika hilo bila kuhusisha wadau wa Dar es Salaam.
Mtemvu alisema mwekezaji anayetajwa alilipa Shilingi milioni 280 na kuhoji hiyo ndiyo thamani ya Uda? Na kwamba shirika hilo hakukabidhiwa na vikao halali bali na Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Katika taarifa yake, Profea Kapuya alisema: “Hakuna dhambi kwa mbunge kufanya biashara, sera inaruhusu na afadhali mimi ninayezunguka kuwaona watu kuliko yeye anayezunguka kwa lengo la kurudisha imprest (masurufu), na anayezungumza ni mmoja wapo.”

Post a Comment